Madhara Ya An-Namiymah (Kufitinisha ) - Vipi Kutibu An-Namiymah?
Mafunzo yafuatayo yataweza Inshaa-Allaah kutibu maovu ya An-Namiymah ikiwa yatatekelezwa na inampasa kila mwenye tabia hii haraka ajifunze ili kujiepusha na maouvu haya yanayosababisha ufisadi na chuki baina ya ndugu Waislamu. Tutambue kuwa hii ni moja wapo ya jihadi ya nafsi kwa kujiepusha na maovu yanayoamrishwa na nafsi, ambayo ni jihadi bora kabisa na itamuweka Muislamu katika Ridhaa Ya Mola wake Mtukufu. Amesema Mtume (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kupitia usimulizi wa Fadhwaalah bin ‘Ubaydullaah (Radhiya Allaahu ‘anhu):
(( ألا أخبركم بالمؤمن؟ من أمنه الناس علىأموالهم وأنفسهم، والمسلم من سلم الناس من لسانه ويده، والمجاهد من جاهد نفسه في طاعة الله، والمهاجر من هجر الخطايا والذنوب)) أحمد والحاكم , قال الألباني "إسناد صحيح" سلسلة الأحاديثالصحيحة
((Je, nikujulisheni kuhusu Muumini? Anayeaminiwa na watu juu ya mali zao na nafsi zao. Na Muislmu anayeweka amani kwa watu kwa ulimi wake na mkono wake. Na mfanyaji jihadi ni yule anayefanya jihadi ya nafsi yake katika kumtii Allaah, na mhamaji Hijrah ni anayehama makosa na madhambi)) [Ahmad, Al Haakim na amesema Al-Albaanyi katika Silisilatul-Ahaadiyth Asw-Swahiyhah: “Hii isnaad Swahiyh]
Mwenye kufitinishwa
1- Inapasa mwenye kuletewa fitna kutahadhari na mfitinishaji kwani mfitinishaji ni fasiki na fasiki anahitaji kukhofiwa hadi upatikane ushahidi kamaasemayo ni kweli. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) (Subhaanahu wa Ta'ala):
((يَا أَيُّهَا الذِينَ آمَنُوا إِنْ جَاءَكُمْ فَاسِقٌ بِنَبَأٍ فَتَبَيَّنُوا أَنْ تُصِيبُوا قَوْمًا بِجَهَالَةٍ فَتُصْبِحُوا عَلَىمَا فَعَلْتُمْ نَادِمِينَ ))
((Enyi mlio amini! Akikujieni mpotovu na khabari yoyote, ichunguzeni, msije mkawasibu watu kwa kutojua, na mkawa tena wenye kujuta kwa mliyoyatenda)) [Al-Hujuraat: 6]
2- Kutokuamini asemayo, uwe na dhana nzuri na nduguyo unayepatana naye, badala ya dhana mbaya kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) (Subhaanahu wa Ta'ala):
((يَا أَيُّهَا الذِينَ آمَنُوا اجْتَنِبُوا كَثِيرًا مِنَ الظَّنِّ إِنَّ بَعْضَ الظَّنِّ إِثْمٌ))
((Enyi mlioamini! Jiepusheni na dhana nyingi, kwani baadhi ya dhana ni dhambi))[Al-Hujuraat: 12]
3- Usipendelee kuwa na urafiki na mfitinishaji na anapokuja kukufitinsha ni vizuri kumpa nasaha, kumkataza asiwe anafanya hivyo hata kama ni kweli kamsikia mwenzako anakusengenya. Kufanya hivi, utakuwa umemfunza yeye kuepukana na tabia hiyo kwani akitambua kuwa wewe sio mtu wa kukubali kupokea ufitinishaji hatorudia tena kwako mara nyingine. Vile vile itakuwa ni kheri kwako kutokusikia tena ufitinishaji na utaepukana na kuwachukia marafiki na ndugu zako ambao una maelewano nao. Kwa ujumla utazuia ufisadi wa aina hii utendeke. Na lau kila mmoja atakuwa anafanya hivi basi bila shaka jamii nzima itaokoka na ufisadi huu wa kufitinisha.
Mwenye kufitinisha
1. Ajishughulishe na kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwa kila aina ya dhikr.
2. Afikirie na akhofu adhabu za kufitinisha.
3. Afikirie ubaya ulioje kuwafitinisha watu na kutia chuki katika nyoyo za watu, je, yeyemwenyewe atapendwa kufitinishwa na kipenzi chake?
4. Asome mada zote za Ghiybah ziliomo humu Fisabillaah.com ili atambue hatari ya kutouhifadhi ulimi.
Mwisho wa mada ya An-Namiymah
Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atuhifadhi na Atuepushe na maovu haya na kila aina ya movu mengine tubakie katika Ridhaa Yake. Aamiyn.
Maoni