Madhara Ya An-Namiymah (Kufitinisha) - Maana, Hukumu Na Adhabu Zake
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
((وَلاَ تُطِعْ كُلَّ حَلاَّفٍ مَّهِينٍ)) ((هَمَّازٍ مَّشَّاء بِنَمِيمٍ)) ((مَنَّاعٍ لِّلْخَيْرِ مُعْتَدٍ أَثِيمٍ))
((Wala usimtii kila mwingi wa kuapa wa kudharauliwa)) ((Mtapitapi, apitaye akifitini)) ((Mwenye kuzuia kheri, dhaalimu, mwingi wa madhambi)) [Al-Qalam: 10-12]
Maana ya An-Namiymah
Ni kufitinisha, kwa maana kuchongeza kwa kuhamisha au kupeleka maneno baina ya watu ili kusababisha wachukiane.
Mfano kumwambia mwenzio: "Fulani kasema kuhusu wewe kadhaa na kadhaa". Au, "Fulani anakuchukia wala hakupendi". Kufitini huku kunaweza kuwa ni kwa kutamka maneno, au kwa kuandika au hata kwa kuonyesha ishara. Kufitinisha kwa kumsingizia mtu au hata kama huyo mtu alisema kweli usemi huo haijuzi kufitinisha.
Mtu kama huyu mwenye kufitinisha ni mwenye nyuso mbili anamkabili kila mmoja kwa uso mzuri kumbe hampendelei kheri, ni kama kinyonga anayebadilika rangi kwa hali anayojipendelea nafsi yake. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametuonya watu kama hawa kwa kusema:
عن أبي هريرة ((إن شر الناس ذو الوجهين الذي يأتي هؤلاء بوجه وهؤلاء بوجه)) البخاري
Kutoka kwa Abu Hurayrah: ((Hakika watu waovu kabisa ni wenye nyuso mbili ambao wanawaendea kundi la watu kwa uso mmoja na kundi la watu wengine kwa uso mwingine)) [Al-Bukhaariy]
Mtu huyu ni tofauti na Muislamu mkweli mwenye uso mmoja katika hali zote baina ya ndugu zake au rafiki zake, naye ana ulimi mmoja wa ukweli, hasemi ila yanaomridhisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
Hukmu ya An-Namiymah
Ni haraam kama ilivyobainishwa katika Qur-aan na Sunnah na miongoni mwa madhambi makubwa.
Athari ya An-Namiymah
Mtafaruku baina ya watu, kuondosha furaha katika nyoyo na badala yake maudhi, kujenga uadui, kuchukiana, kukatiana au kuzuiliana rizki, na huenda ikasabisha hata kuuana.
عن ابن مسعود رضي الله عنه أن النبي "صلى الله عليه وسلم "قال : ((ألا أنبئكم ما العضه؟ هي النميمة القالة بين الناس)) رواه مسلم
Kutoka kwa Ibn Mas'uud (Radhiya Allaahu 'anhu) ambaye amesimulia kwamba: Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Je, nikujulisheni nini Al-'Adhwhu? Ni kuchongeza baina ya watu)) [Muslim]
Adhabu zake
Kuharamishwa Pepo:
عن حذيفة رضي الله عنه قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: ((لا يَدْخُلُ الجَنَّةَ نَمَّامٌ)) رواه البخاري ومسلم
Kutoka kwa Hudhayfah (Radhiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema: Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mchongezi hataingia Peponi))[Al-Bukhaariy na Muslim]
Adhabu Kaburini
عن ابن عباس رضي الله عنهما أن رسول الله صلى الله عليه وسلم مر بقبرين فقال ((إنهما يعذبان, وما يعذبان في كبير, بلى إنه كبير: أما أحدهما كان يمشي بالنميمة و أما ألأخر فكان لا يستتر من بوله)) متفق عليه
Kutoka kwa Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu 'anhuma) ambaye amesimulia kwamba: Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliyapitia makaburi mawili na akasema: ((Hakika hawa wanaadhibiwa. Wala hawaadhibiwi kwa sababu ya jambo kubwa. Ndio ni jambo kubwa! Mmoja wao alikuwa akipita kuchongeza na mwingine alikuwa hajikingi na mkojo [anapokojoa]))[Al-Bukhaariy na Muslim]
Inaendelea
Maoni