Ruka hadi kwenye maudhui makuu

Kutengukwa Na Wudhuu Katika Swalah Ya Jamaa

SWALI

Kama unasali jamaa kati kati ukatengukwa na udhu utahitajika kuondoka pale pale au usubiri umalize then utie udhu usali tena? ukizingatia jamii yetu wengi hatujui namna ya kupishana katika sala ukitokewa na udhuru.

 

JIBU

 
 Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Swalah hili ni muhimu  na linahitaji kuonyeshwa kimatendo kwani huenda lisifahamike katika waraka. Hivyo, itabidi katika Misikiti watu wafundishwe ili kusiwe na utata aina yoyote baada ya hapo. Kwani hili ni tatizo kubwa katika jamii zetu kujua namna ya kutoka pindi mtu anapotengukwa na wudhuu. Lakini Insha’Allah tujaribu na tunamuomba Allah atupatie tawfiki katika hilo. Pindi wudhuu unapovunjika inakuwa huwezi tena kuendelea na Swalah na inabidi uondoke ili ukachukue wudhuu na urudi uanze Swalah ile kuanzia mwanzo.

 

Wudhuu unapomtenguka mmoja wetu inabidi akate Swalah na aanze harakati za kutoka ili aende kuchukua wudhuu mpya. Hapo atasimama nyuma ya mtu wa upande wa kushoto au kuumeni katika wale waliokuwa naye msitari mmoja. Na anaweza kumuashiria yule aliye katika msitari wa nyuma ili ajongee katika nafasi yake. yeye naye atapiga hatua katika ile nafasi iliyoachwa wazi kwa yule wa nyuma kujongea mbele. Atasimama tena nyuma ya mtu wa msitari huu wa nyuma. Huyu wa msitari wa tatu atakuja kuziba ule mwanya na ataendelea hivyo mpaka afike sehemu ya kuchukua wudhuu. Akiona kuwa kutoka kwake kunaweza kuleta shida zaidi na vurugu kwa wengine au kuleta tashwishi ya kuwaondolea khushuu wengine, itakuwa ni afadhali abakie amekaa katika sehemu yake mpaka jamaa imalizike kisha atoke kwenda kuchukua wudhuu mpya kwa ajili ya kuanza Swalah upya.

 

Lakini pia kuna ushahidi mwengine uuoneshao kuwa mtu anaweza kupita mbele ya safu nyuma ya Imaam na hatokuwa amewakata wenzake Swalah, kwani katika Sahihi Al Bukhariy,

 

(( سترة الإمام سترة من خلفه))  البخاري

((Sutra ya Imaam ni Sutra ya walio nyuma yake)) Al-Bukhariy

 

 

Na maadam Maamuma kizuizi chao ni kile kizuizi cha Imaam, basi haikatwi Swalah yao kwa kupita mtu mbele yaokama tunavyoona katika tukio la Ibn ‘Abbaas رضي الله عنهما:

 

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عَبَّاسٍ رضي الله عنهما قَالَ : أَقْبَلْتُ رَاكِباً عَلَى حِمَارٍ أَتَانٍ , وَأَنَا يَوْمَئِذٍ قَدْ نَاهَزْتُ الاحْتِلامَ وَرَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم يُصَلِّي بِالنَّاسِ بِمِنًى إلَى غَيْرِ جِدَارٍ، فمَرَرْتُ بَيْنَ يَدَيْ بَعْضِ الصَّفِّ فَنَزَلْتُ, فَأَرْسَلْتُ الأَتَانَ تَرْتَعُ، وَدَخَلْتُ فِي الصَّفِّ  فَلَمْ يُنْكِرْ ذَلِكَ عَلَيَّ أَحَدٌ .

 

Imetoka kwa Ibn ‘Abbaas  رضي الله عنهماambaye kasema: “Nilikuja siku moja huku nimepanda punda mwanamke na nilikuwa ndio kwanza nafikia umri wa kubaleghe, Na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم   anaswalisha watu huko Minaa bila ya kuweko ukuta mbele yake. Nikapita baina ya baadhi ya safu, kisha nikateremka, nikampeleka punda (sehemu ya ) kumlisha, na nikaingia katika safu, wala hakuniambia mtu lolote kuhusu hivyo nilivyofanya”  Al-Bukhariy

 

 

Na katika hadithi nyingine iliyosimuliwa na Imaam Muslim

 

من طريق عبيد الله بن عبد الله بن عتبة أن عبد الله بن عباس أخبره أنه أقبل يسير على حمار ورسول الله صلى الله عليه وسلم قائم يصلي بِمِنى في حجة الوداع، يُصلي بالناس. قال : فَسَارَ الحمار بين يدي بعض الصف، ثمنزل عنه ، فَصَفّ مع الناس.

 

Na katika Hadithi iliyosimuliwa na Muslim kupitia kwa 'Ubaydullaah bin Abdullaah bin 'Utbah kwamba Abdullaah bin 'Abbaas kamjulisha kuwa alifika huku kapanda punda na Mtume   صلى الله عليه وآله وسلم kasimama anaswalisha watu alipokuwa Minaa katika Hijjatul Widaa. Akasema:  Akawa anapita na punda baina ya safu, kisha akateremka akaingia katika safu (kuswali) pamoja na watu”   

 

 

Hadithi hizi zinatujulisha kuwa mtu anaweza kupita mbele ya safu za Maamuma kama kuna haja ya kufanya hivyo, na bila ya kuwa na makatazo yoyote juu ya hilo. Pia kuna hadithi kama hizo iliyopo kwenye Sahih Muslim ambayo Ibn ‘Abbaas رضي الله عنهما anasimulia kuwa alikuwa na nduguye juu ya kipando na wakapita mbele ya safu na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم   hakuwaambia chochote.

 

 

Pia tunaona katika hadithi hizi kuwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  aliswali bila ya kuweko na ukuta mbele yake, kwa hiyo Swalah ya Maamuma ni kumfuata Imaam hata kama Imaam hana sutra mbele yake, na haidhuru ikiwa mtu atapita baina ya safu, kwa maana kuwa huyo mtu haikati Swalah za wanaoswali. Vile vile ingawa katika hadithi nyingine ya sahihi inayosema kuwa miongoni mwa vitu vinavyoharibu Swalah ni kupita kwa punda ikiwa atapita mbele ya Imaam au mtu anayeswali pekee, lakini hapa haikuharibu Swalah kupita punda baina ya safu.  

 
Wa Allaahu A'alam

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Hukumu ya kupeleka barua ya posa kwenye kitambaa cheupe

                      Hukumu ya kupeleka barua ya posa kwenye kitambaa cheupe  Hakika ni kuwa posa ilivyofanyika katika Uislamu kuanzia wakati wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) inafahamika vilivyo. Posa inaweza kuja kutoka kwa mume na watu wake kwa jamaa za mke au mzazi wa mke kumtafutia binti yake mume. Ikiwa wazazi watakwenda kwa wazazi wa mke, baada ya kupeleka maneno, na wazazi wa mke watataka kupatiwa muda wa kufikiria, kufanya shuuraa, kuulizia, kutafiti na baadaye kukubali au kukataa. Ikiwa wamekubali baada ya kumshauri binti  yao  ni vyema mume mtarajiwa aende amuone atakaye kuwa mkewe ili apate kutulia na kuridhika kabla siku ya Nikaah. Binti huyo au wazazi wake wataweka kiwango cha mahari ambacho mume anatakiwa kutoa. Hii njia ya kuweka pesa kwenye kitambaa au bahasha haipo katika mafunzo ya Kiislam, na huenda ni njia ya kitamaduni fulani au itikadi f...

Maana ya Uadilifu

                                         MAANA  YA  UADILIFU  KATIKA  UISLAMU Assallaam  Aleykum  WarahmatulLaah  Wabarakatuh Alhamdu Lillaahi Rabil'aalamiyn) Allaahumma Swalli 'alaa Muhammad wa 'alaa aali Muhammad kamaa Swallayta 'alaa Ibraahiym wa 'alaa aali Ibraahiym wa Baarik 'alaa Muhammad wa 'alaa aali Muhammad kamaa Baarakta 'alaa Ibraahiym wa 'alaa aali Ibraahiym fil'aalamyna Innaka Hamiydun Majiyd. Ndugu zangu Waislam Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema katika Qur-aan. إِنَّ اللَّـهَ يَأْمُرُ بِالْعَدْلِ وَالْإِحْسَانِ وَإِيتَاءِ ذِي الْقُرْبَىٰ وَيَنْهَىٰ عَنِ الْفَحْشَاءِ وَالْمُنكَرِ وَالْبَغْيِ ۚيَعِظُكُمْ لَعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ Hakika Allaah Anaamrishia uadilifu na ihsaan na kuwapa (mahitajio na msaada) jamaa wa karibu; na Anakataza machafu na munkari na ukandamizaji. Anakuwaidhini huenda mkapata kukumb...

Viungo vya Mwili vitashuhudia Matendo ya Mwanaadamu Siku ya Qiyaamah

Anasema Allaah  سبحانه وتعالى   ((الْيَوْمَ نَخْتِمُ عَلَى أَفْوَاهِهِمْ وَتُكَلِّمُنَا أَيْدِيهِمْ وَتَشْهَدُ أَرْجُلُهُمْ بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ)) ((Leo Tunaviziba vinywa vyao, na iseme Nasi mikono  yao , na itoe ushahidi miguu  yao kwa waliyokuwa wakiyachuma))  [Yaasiyn :65 ] Siku ya Qiyaamah viungo vya miili vitakuwa ni vyenye kushuhudia matendo ya binaadamu aliyoyatenda hapa duniani: Mfano mikono itasema: "nimeiba".  Miguu itasema, "nimekwenda sehemu ya ma'asi". Macho yatasema, "nimetazama machafu".  Masikio yatasema, "nimesikiliza nyimbo, au umbea" na kadhalika. Na hivi ndivyo itakavyokuwa hali ya makafiri, wanafiki na wenye kumuasi Mola siku ya kufufuliwa,  watakapokanusha madhambi waliyoyatenda duniani na kuapa kwamba hawakuyafanya, Allaah  سبحانه وتعالى  Atawafunga midomo  yao na kuviamrisha viungo vizungumze:   عن أنس بن مالك قال: كنا عند النبي صلى ال...