Hukumu ya swalah ya ´Iyd
Ndugu muislamu! Jifunze baadhi ya hukumu muhimu unazotakiwa kuzijua zinazohusiana na mwezi huu mtukufu.
Swalah ya ´Iyd
Kwa mujibu wa wanachuoni wengi swalah ya ´Iyd ni faradhi kwa baadhi ya waislamu. Inajuzu kwa baadhi kutoiswali. Hata hivyo imependekezwa kuihudhuria na mtu kushirikiana na ndugu zake waislamu. Ni Sunnah iliyokokotezwa isiyotakikana kuachwa isipokuwa kwa kuwepo udhuru wa Kishari´ah.
Baadhi ya wanachuoni wanaonelea kuwa ni lazima kwa waislamu wote kuiswali kama swalah ya Ijumaa. Wanaume wote katika mji na ambao wana majukumu juu ya matendo yao ni lazima waiswali. Maoni haya ndio yanaonekana kuwa dalili yenye nguvu na ilio karibu zaidi na usawa.
Ni Sunnah kwa wanawake kuihudhuria. Lakini wanatakiwa kuzingatia kujisitiri vizuri na kutojitia manukato. Imethibiti kwa al-Bukhaariy na Muslim ya kwamba Umm ´Atwiyyah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:
“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametuamrisha kuwatoa nje siku ya ´Iyd mbili wanawake vijana ambao ndio karibuni wametoka kukomaa, wanawake wenye hedhi na mabikira. Kuhusiana na wanawake wenye hedhi, wajitenge mbali na kuswali.”[1]
Katika upokezi mwingine imekuja:
“Ee Mtume wa Allaah! Mmoja wetu hana Jilbaab ya kutoka nayo?” Akasema: “Dada yake ampe moja katika Jilbaab zake.””[2]
Ni jambo lisilo na shaka ya kwamba haya yanafahamisha kuwa imekokotezwa kwa wanawake kutoka na kuswali swalah za ´Iyd na washiriki kheri na du´aa ya waislamu.
Lililo Sunnah kwa anayefika mahala pa kuswalia swalah ya ´Iyd au swalah ya mvua akae moja kwa moja na wala asiswali Rakaa´ mbili za Sunnah kwanza. Kutokana na ninavyojua kitu kama hicho hakikupokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala Maswahabah zake (Radhiya Allaahu ´anhum). Isipokuwa tu ikiwa inaswaliwa msikitini. Katika hali hii atatakiwa kuswali Rakaa´ mbili za Sunnah kutokana na jumla ya maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):
“Mmoja wenu atapoingia msikitini asikae mpaka kwanza aswali Rakaa´ mbili.”[3]
Kwa ambaye amekaa na kusubiri swalah ya ´Iyd imewekwa katika Shari´ah akithirishe kusema “Laa ilaaha illa Allaah” na “Allaahu Akbar”. Ni nembo ya siku hiyo. Ni Sunnah kwa wote waliyoko ndani ya msikiti na nje ya msikiti mpaka Khutbah itapoisha. Ni sawa vilevile kujishughulisha na kusoma Qur-aan.
Napendelea kuweka wazi kwamba asli Takbiyr inatakiwa kutamkwa usiku wa ´Iyd na kabla ya swalah ya ´Iyd pamoja vilevile na yale masiku kumi ya mwanzo ya Dhul-Hijjah na masiku ya Tashriyq. Imewekwa katika Shari´ah kwenye masiku haya matukufu. Ndani yake mna fadhila tele kutokana na maneno ya Allaah (Ta´ala) juu ya Takbiyr katika mnasaba wa ´Iyd baada ya Ramadhaan:
وَلِتُكْمِلُوا الْعِدَّةَ وَلِتُكَبِّرُوا اللَّـهَ عَلَىٰ مَا هَدَاكُمْ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ
“… na ili mkamilishe idadi na ili mumkabiri Allaah kwa kuwa amekuongozeni na mpate kushukuru.”[4]
Allaah (Ta´ala) amesema pia kuhusu yale masiku kumi ya mwanzo ya Dhul-Hijjah na masiku ya Tashriyq:
لِّيَشْهَدُوا مَنَافِعَ لَهُمْ وَيَذْكُرُوا اسْمَ اللَّـهِ فِي أَيَّامٍ مَّعْلُومَاتٍ عَلَىٰ مَا رَزَقَهُم مِّن بَهِيمَةِ الْأَنْعَامِ ۖ فَكُلُوا مِنْهَا وَأَطْعِمُوا الْبَائِسَ الْفَقِيرَ
“… ili washuhudie manufaa yao na walitaje Jina la Allaah katika siku maalumu kwa yale aliyowaruzuku kati ya wanyama wenye miguu minne wa mifugo. Basi kuleni humo na lisheni mwenye shida fakiri.”[5]
Allaah (´Azza wa Jall) amesema vilevile:
وَاذْكُرُوا اللَّـهَ فِي أَيَّامٍ مَّعْدُودَاتٍ
“Mdhukuruni Allaah katika siku za kuhesabika.”[6]
Katika masiku haya maalum na yaliyotengwa imewekwa katika Shari´ah kumdhukuru Allaah kwa Takbiyr ambazo hazikufungamana na zilizofungamana. Ni jambo lina asli katika Sunnah twaharifu na matendo ya Salaf. Njia ya Takbiyr iliyowekwa katika Shari´ah ni kila muislamu kusema “Allaahu Akbar” kivyake. Anatakiwa kunyanyua sauti yake kiasi cha kwamba wengine waweze kumsikia ili wamuige na wadhukuru kupitia yeye. Kuhusu Takbiyr za kwa pamoja na zilizozuliwa, ni watu wasiopungua wawili wanyanyue sauti zao za Takbiyr kwa njia ya kwamba wanaanza na kumaliza kwa pamoja na wanafanya hivo kwa sauti ya pamoja na kwa njia maalum. Kitendo hichi hakina asli wala hakina dalili. Ni uzushi. Allaah hakuteremsha dalili yoyote juu ya hilo.
´Iyd ikiangukia siku ya Ijumaa ambaye ameswali swalah ya ´Iyd ana khiyari ya kuswali swalah ya Ijumaa au Dhuhr. Imethibiti kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:
“Leo zimekutana sikukuu mbili. Aliyeswali ´Iyd hahitajii kuswali Ijumaa.”[7]
Lakini hatakiwi kuacha kuswali Dhuhr. Lililo bora ni yeye kuswali swalah ya Ijumaa pamoja na wengine. Iwapo hatoswali swalah ya Ijumaa anatakiwa badala yake kuswali Dhuhr.
Kuhusu imamu anatakiwa kuswali swalah ya Ijumaa pamoja na wale waliohudhuria wakiwa hawapungui watu watatu pamoja na imamu. Endapo hakutohudhuria isipokuwa mtu mmoja tu ataswali Dhuhr pamoja naye.
Ni sawa kwa muislamu kumwambia ndugu yake siku ya ´Iyd au siku nyengine:
“Allaah atukubalie sisi na nyinyi matendo yetu mema.”
[1] al-Bukhaariy (324) na Muslim (890).
[2] Muslim (890).
[3] al-Bukhaariy (1167) na Muslim (714).
[4] 02:185
[5] 22:28
[6] 02:203
[7] Abu Daawuud (1073) na Ibn Maajah (1311). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Abiy Daawuud” (948).
Maoni