Ruka hadi kwenye maudhui makuu

Watu ambao Allaah hatowatizama wala Kuongea nao siku ya Qiyamah - sehemu ya 1

                   Watu ambao Allaah hatowatizama wala Kuongea nao siku ya Qiyamah.



Hadiyth ya Kwanza

Mzee Mzinzi, Mfalme Mwongo, na Masikini Mwenye Kibri


 عن أبي هريرة قال: قال رسول الله صلى اللهعليه وسلم: ((ثلاثةٌ لا يكلمهم الله يومالقيامة، ولا يزكيهم، ولا ينظر إليهم، ولهمعذابٌ أليمٌ: شيخٌ زانٍ، وملكٌ كذابٌ، وعائلٌمستكبرٌ))  رواه مسلم.
Imepokelewa toka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Wa tatu, Allaah Hatozungumza nao Siku ya Qiyaamah, wala Hatawatakasa, wala Hatawaangalia, na watapata adhabu iumizayo: Mzee mzinzi, mfalme mwongo, na masikini mwenye kibri)). [Imesimuliwa na Muslim]


Faida na Sharh ya Hadiyth.

Makusudio ya Allaah ('Azza wa Jalla)  kutozungumza nao ni kuwa Hatozungumza nao mazungumzo ya kuwa radhi nao na kuwafurahikia, bali Atazungumza nao mazungumzo ya hasira na kutowafurahikia.

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Anasifika na sifa hii ya kuzungumza. Huzungumza wakati wowote Atakapo na kwa namna yoyote Aitakayo. Alizungumza na Nabiy Muwsaa ('Alayhis-Salaam)  Akazungumza na Nabiy wetu Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  usiku wa Mi’iraaj, na pia Atazungumza na Nabiy ‘Iysaa  ('Alayhis-Salaam)  Siku ya Qiyaamah Amuulize:

   وَإِذْ قَالَ اللَّـهُ يَا عِيسَى ابْنَ مَرْيَمَ أَأَنتَ قُلْتَ لِلنَّاسِ اتَّخِذُونِي وَأُمِّيَ إِلَـٰهَيْنِ مِن دُونِ اللَّـهِ ۖ قَالَ سُبْحَانَكَ مَا يَكُونُ لِي أَنْ أَقُولَ مَا لَيْسَ لِي بِحَقٍّ ۚ إِن كُنتُ قُلْتُهُ فَقَدْ عَلِمْتَهُ ۚ تَعْلَمُ مَا فِي نَفْسِي وَلَا أَعْلَمُ مَا فِي نَفْسِكَ ۚ إِنَّكَ أَنتَ عَلَّامُ الْغُيُوبِ  
((Na pindi Allaah Atakaposema: “Ee ‘Iysaa mwana wa Maryam!  Je, wewe uliwaambia watu: ‘Nifanyeni mimi na mama yangu kuwa ni waabudiwa wawili badala ya Allaah?” (‘Iysaa) Atasema: “Utakasifu ni Wako hainipasi mimi kusema yasiyo kuwa haki kwangu; ikiwa nimesema hayo basi kwa yakini Ungeliyajua; Unayajua yale yote yaliyomo katika nafsi yangu; na wala mimi sijui yale yaliyomo katika Nafsi Yako; hakika Wewe ni Mjuzi wa ghayb)). [Al-Maaidah (5:116)]

Aidha, Atazungumza mazungumzo makali ya hasira na magombesho kwa makafiri na waasi Siku ya Qiyaamah. Atawaambia watu wa motoni kwa mfano:

قَالَ اخْسَئُوا فِيهَا وَلَا تُكَلِّمُونِ ﴿١٠٨﴾
108. Wataambiwa: “Hizikeni humo! Na wala msinisemeshe!”   [Al-Muuminuwn: 108]


Ama kutakaswa,  ni kutwaharishwa. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Huwatwaharisha  Waja Wake wema hapa duniani kwa kuzizidishia nyoyo zao iymaan, matendo mema na taqwa. Anatuambia:
قَدْ أَفْلَحَ مَن تَزَكَّىٰ ﴿١٤﴾
14. Hakika amefaulu ambaye amejitakasa.


وَذَكَرَ اسْمَ رَبِّهِ فَصَلَّىٰ ﴿١٥﴾
15. Na akadhukuru Jina la Rabb wake na akaswali. [Al-A’laa: 14-15]


Na huko Aakhirah inakuwa kwa kuwasafisha kutokana na uchafu wa makosa wakatakata kabisa na kisha kuwaingiza Peponi, kwani Peponi haingii mtu mchafu.

Ama kuwaangalia, makusudio yake ni kuwaangalia kwa jicho la ridhaa na furaha. Kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anawaangalia viumbe Vyake vyote bila kukiacha hata kimoja.

Watu hao watakaokumbana na mkasa huu:

Mtu wa kwanza: Mzee, ajuza na kikongwe mzinifu na mzinzi. 

Mzee kama huyu ambaye umri wake umesonga mbele, anachotakiwa ni kujikurubisha zaidi kwa Allaah ('Azza wa Jalla)  badala ya kumwasi kwa kosa hili ambalo Allaah ('Azza wa Jalla)  Amelielezea kama ni uchafu na njia mbaya kabisa. Mzee kama huyu inaonyesha kwamba mizizi ya madhambi imejikita hadi kwenye kina cha mwisho cha moyo wake.


Mtu wa pili: Ni mfalme mwongo.

Mwana Aadam kawaida husema uongo kutokana na unyonge wake na udhaifu wake na kushindwa kuwakabili wenye nguvu kwa haki na ukweli, na hapo hulazimika kuongopa. Ama mfalme, yeye anamwogopa nani? 

Watu wote ni raia wake, na vyombo vyote vya dola viko chini yake. Na ikiwa anaongopa, basi ni dalili kuwa mfalme huyo ni mchafu kimaadili, fisadi, mwenye uchu, na ubaya wa kila aina umejikita ndani ya nafsi yake.

Hii ni kama mzazi kuwaongopea watoto wake. Ni kwa nini afanye hivyo? 

Anaweza kuwaambia ukweli kwenye kila kitu, nao wakafahamu, wakavaana na hali iliyopo na wakakulia katika mazingira ya usemaji kweli. Na baba anapowaongopea watoto, inakuwa ni dhambi kubwa ambalo wengi hawalihisi. 

Na baba huyu anaweza kuwa sawa na mfalme huyo, na akaingia kwenye makamio haya ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).


Mtu wa tatu: Ni masikini jeuri mwenye kibr.

Kibr mara nyingi huchochewa na utajiri alionao mtu ambapo watu hujipendekeza kwake na kumwonyesha kuwa wanamheshimu na kumtukuza kwa ajili ya maslaha. Hali hii mara nyingi humfanya mtu kuwa na kibr. Allaah ('Azza wa Jalla)  Anatuambia:
((كَلَّا إِنَّ الْإِنسَانَ لَيَطْغَىٰ))
((Laa hasha! Hakika mwana Aadam bila shaka amepindukia mipaka kuasi ))
((أَن رَّآهُ اسْتَغْنَىٰ ))
((Kwa kuwa amejiona amejitosheleza)) [Al-‘Alaq 96: 6 - 7]


Basi ikiwa mtu masikini na mlalahoi, na akawa na kibr, hii bila shaka inaonyesha kuwa uovu na uhabithi umejikita ndani ya nafsi yake. Mtu huyu bila shaka anaishi maisha ya taabu, dhiki na kubahatisha hapa duniani, na huko Aakhirah atakwenda kukumbana na makamio hayo ya Allaah (‘Azza wa Jalla). Anakuwa amekhasirika hapa duniani na huko aakhirah.

مستكبر anaweza pia kuwa mtu anayependa kujionyesha kwa watu kinyume na uwezo wake. Anaweza hata kuazima nguo, au kununua kitu cha ghali kwa kukopa, au kufanya harusi kubwa kwa madeni, ili tu mradi aonekane na yeye ni katika watu wa hadhi ya juu nailhali hana chochote. Hili wanalo wengi sana katika jamii.

Au hata akina mama wanapoalikwa kwenye harusi na kadhalika, hujitahidi kununua nguo ya ghali isiyopatikana nchini mwake na kuiagizia nje ili tu aonekane yeye tu aliyevaa nguo hiyo pasina mwengine.


Na  Allaah  anajua zaidi

Inaendelea usikose sehemu ya 2 In Shaa Allaah.....................

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Hukumu ya kupeleka barua ya posa kwenye kitambaa cheupe

                      Hukumu ya kupeleka barua ya posa kwenye kitambaa cheupe  Hakika ni kuwa posa ilivyofanyika katika Uislamu kuanzia wakati wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) inafahamika vilivyo. Posa inaweza kuja kutoka kwa mume na watu wake kwa jamaa za mke au mzazi wa mke kumtafutia binti yake mume. Ikiwa wazazi watakwenda kwa wazazi wa mke, baada ya kupeleka maneno, na wazazi wa mke watataka kupatiwa muda wa kufikiria, kufanya shuuraa, kuulizia, kutafiti na baadaye kukubali au kukataa. Ikiwa wamekubali baada ya kumshauri binti  yao  ni vyema mume mtarajiwa aende amuone atakaye kuwa mkewe ili apate kutulia na kuridhika kabla siku ya Nikaah. Binti huyo au wazazi wake wataweka kiwango cha mahari ambacho mume anatakiwa kutoa. Hii njia ya kuweka pesa kwenye kitambaa au bahasha haipo katika mafunzo ya Kiislam, na huenda ni njia ya kitamaduni fulani au itikadi f...

Maana ya Uadilifu

                                         MAANA  YA  UADILIFU  KATIKA  UISLAMU Assallaam  Aleykum  WarahmatulLaah  Wabarakatuh Alhamdu Lillaahi Rabil'aalamiyn) Allaahumma Swalli 'alaa Muhammad wa 'alaa aali Muhammad kamaa Swallayta 'alaa Ibraahiym wa 'alaa aali Ibraahiym wa Baarik 'alaa Muhammad wa 'alaa aali Muhammad kamaa Baarakta 'alaa Ibraahiym wa 'alaa aali Ibraahiym fil'aalamyna Innaka Hamiydun Majiyd. Ndugu zangu Waislam Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema katika Qur-aan. إِنَّ اللَّـهَ يَأْمُرُ بِالْعَدْلِ وَالْإِحْسَانِ وَإِيتَاءِ ذِي الْقُرْبَىٰ وَيَنْهَىٰ عَنِ الْفَحْشَاءِ وَالْمُنكَرِ وَالْبَغْيِ ۚيَعِظُكُمْ لَعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ Hakika Allaah Anaamrishia uadilifu na ihsaan na kuwapa (mahitajio na msaada) jamaa wa karibu; na Anakataza machafu na munkari na ukandamizaji. Anakuwaidhini huenda mkapata kukumb...

Hukumu ya Wudhuu kwa mwaamke aliyepaka kucha rangi

Swali:  Ni ipi hukumu ya wudhuu´ kwa yule ambaye kwenye kucha zake amepaka rangi ya kucha? Jibu:  Rangi ya kucha ni kitu anachopaka mwanamke juu ya kucha na ni kitu kilicho na ukoko.  Kwahiyo haijuzu kwa mwanamke kuitumia kipindi ambapo anaswali kwa kuwa inazuia maji kufika kwenye ngozi wakati wa kutawadha.  Kila kitu kinachozuia maji kufika kwenye ngozi haijuzu kwa mwenye kutawadha kukitumia. Kwa kuwa Allaah amesema: فَاغْسِلُوا وُجُوهَكُمْ وَأَيْدِيَكُمْ “Hivyo basi osheni nyuso zenu na mikono yenu mpaka kwenye visugudi.” (05:06) Mwanamke huyu ambaye amepaka juu ya kucha zake rangi ya kucha yanazuia maji kufika kwenye ngozi.  Kwa hivyo hawezi kusadikishwa ya kwamba ameosha mikono. Katika hali hiyo anakuwa ameacha kiungo cha faradhi wakati wa kutawadha au wakati wa kuoga. Kuhusu wale wasioswali, kama mfano wa mwanamke mwenye hedhi, hakuna neno kuitumia. Isipokuwa ikiwa kama rangi hii ni katika mambo maalum ya makafir...