Ruka hadi kwenye maudhui makuu

Mke amefariki hali ya kuwa hajamaliza mahari, Je mke atakaa eda na kukamilisha Mahari?

*Swali*

Mume ameoa siku ya Ijumaa, na akadhamiria kumfuata mkewe siku ya jumapili, ila kwa Qadar ya Allaah yule Mume akafariki Siku ya Jumamos na hali ya kua hajamaliza Mahari, na wala hajamuingilia mkewe.

1.Je,mke huyo ipo haja amaliziwe mahari yake  au yeye mke ndio arejeshe Mahari?

2.Je mke atakaa Eda?  Na ni Eda gani?

3.Je,mke huyo atarithi kwa Mumewe aliyefariki? 

*Majibu*

Bismillaahir Rahmaniir Rahiim

Kwanza kabisa shukrani kwa Swali lako, ila kwanza kabla sijakujibu swali lako naomba mjihadhali sana na Maswali ya kutunga.

Mke atakamilishiwa mahari yake kamili.

Ibn Mas'uwd (Radhwiya Allaahu 'anhu) aliulizwa kuhusu mwanamme ambaye alimuoa mwanamke na hakutaja mahari yake au kumuingilia kabla ya kufa (mwanamme). Ibn Mas'uwd (Radhwiya Allaahu 'anhu) akajibu: "Anapaswa kupewa mahari yake kama wanawake mfano wake; si ziada wala pungufu, na vilevile anapaswa kukaa eda, na ana haki ya Miyraath.

Ma'quwl bin Sinaan Al-Ashja'iy (Radhwiya Allaahu 'anhu) alisimama (baada ya kusikia hukmu (fatwa) ya suala hilo kutoka kwa Ibn Mas'uwd) na kusema: Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitoa hukmu kuhusiana na Birwa' bint Waashiq, mmoja katika wanawake wetu, na hiyo hukmu (fatwa) ilikuwa kama ambayo umeitoa wewe.

Ibn Mas'uwd (Radhwiya Allaahu 'anhu) alifurahi kwa habari (taarifa) hiyo (ya kufahamishwa kuwa hukmu yake imewafikiana na hukmu iliyowahi kutolewa na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

[At-Tirmidhiy, na amesema Shaykh Al-Albaaniy kuwa ni sahihi katika Swahiyh Sunan At-Tirmidhiy]

Mke atakaa eda ya kufiwa sawa na mwanamke aliyeingiliwa.

Atakaa eda kama mwanamke yeyote mwengine aliyefiwa na mumewe; ikiwa hajaingiliwa au ameingiliwa kabla ya mume kufariki.

Na hiyo ni kwa ujumla wa maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alivyosema:

وَالَّذِينَ يُتَوَفَّوْنَ مِنكُمْ وَيَذَرُونَ أَزْوَاجًا يَتَرَبَّصْنَ بِأَنفُسِهِنَّ أَرْبَعَةَ أَشْهُرٍ وَعَشْرًا ۖ ... ﴿٢٣٤﴾

Na wale wanaofishwa miongoni mwenu na wakaacha wake, hao wake wangojee peke yao (eda) miezi minne na siku kumi...

[Al-Baqarah: 234].

Na dalili nyingine ni riwaaya ya Ibn Mas'uwd (Radhwiya Allaahu 'anhu).

Kwa faida ya nyongeza, ikiwa mwanamke alipewa talaka kabla hajaingiliwa na mumewe, basi huyo hatokaa eda kwa dalili ya maneno Yake Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نَكَحْتُمُ الْمُؤْمِنَاتِ ثُمَّ طَلَّقْتُمُوهُنَّ مِن قَبْلِ أَن تَمَسُّوهُنَّ فَمَا لَكُمْ عَلَيْهِنَّ مِنْ عِدَّةٍ تَعْتَدُّونَهَا ۖ ... ﴿٤٩﴾

Enyi walioamini! Mnapofunga nikaah na Waumini wa kike, kisha mkawataliki kabla ya kujimai nao,hamna juu yao eda yoyote mtakayohesabu…  [Al-Ahzaab: 49]

Hii ni dalili ya kuthibitisha kuwa mwanamke aliyepewa talaka bila kuingiliwa (bila kufanyika Jimaa') hatokaa eda kwa makubaliano ya Wanachuoni.

Ama mwanamke ambaye alikuwa kaishaingiliwa na mumewe kisha akapewa talaka, huyo atakaa eda kwa makubaliano ya Wanachuoni vilevile.

Mke atamrithi mume aliyefariki hata ikiwa hakuwahi kuingiliwa.

Na kiwango cha Miyraath kinategemea na hali aliyokuwa nayo mume aliyefariki. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

... وَلَهُنَّ الرُّبُعُ مِمَّا تَرَكْتُمْ إِن لَّمْ يَكُن لَّكُمْ وَلَدٌ ۚ فَإِن كَانَ لَكُمْ وَلَدٌ فَلَهُنَّ الثُّمُنُ مِمَّا تَرَكْتُم ۚ مِّن بَعْدِ وَصِيَّةٍ تُوصُونَ بِهَا أَوْ دَيْنٍ ۗ ... ﴿١٢﴾

...Nao wake zenu watastahiki robo katika mlichoacha ikiwa hamna mtoto. Na ikiwa mna mtoto basi watastahiki thumni katika mlichoacha, baada ya kutoa wasia mliousia au kulipa deni...

[An-Nisaa: 12]

Na Allaah ni Mjuzi zaidi.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Hukumu ya kupeleka barua ya posa kwenye kitambaa cheupe

                      Hukumu ya kupeleka barua ya posa kwenye kitambaa cheupe  Hakika ni kuwa posa ilivyofanyika katika Uislamu kuanzia wakati wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) inafahamika vilivyo. Posa inaweza kuja kutoka kwa mume na watu wake kwa jamaa za mke au mzazi wa mke kumtafutia binti yake mume. Ikiwa wazazi watakwenda kwa wazazi wa mke, baada ya kupeleka maneno, na wazazi wa mke watataka kupatiwa muda wa kufikiria, kufanya shuuraa, kuulizia, kutafiti na baadaye kukubali au kukataa. Ikiwa wamekubali baada ya kumshauri binti  yao  ni vyema mume mtarajiwa aende amuone atakaye kuwa mkewe ili apate kutulia na kuridhika kabla siku ya Nikaah. Binti huyo au wazazi wake wataweka kiwango cha mahari ambacho mume anatakiwa kutoa. Hii njia ya kuweka pesa kwenye kitambaa au bahasha haipo katika mafunzo ya Kiislam, na huenda ni njia ya kitamaduni fulani au itikadi f...

Maana ya Uadilifu

                                         MAANA  YA  UADILIFU  KATIKA  UISLAMU Assallaam  Aleykum  WarahmatulLaah  Wabarakatuh Alhamdu Lillaahi Rabil'aalamiyn) Allaahumma Swalli 'alaa Muhammad wa 'alaa aali Muhammad kamaa Swallayta 'alaa Ibraahiym wa 'alaa aali Ibraahiym wa Baarik 'alaa Muhammad wa 'alaa aali Muhammad kamaa Baarakta 'alaa Ibraahiym wa 'alaa aali Ibraahiym fil'aalamyna Innaka Hamiydun Majiyd. Ndugu zangu Waislam Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema katika Qur-aan. إِنَّ اللَّـهَ يَأْمُرُ بِالْعَدْلِ وَالْإِحْسَانِ وَإِيتَاءِ ذِي الْقُرْبَىٰ وَيَنْهَىٰ عَنِ الْفَحْشَاءِ وَالْمُنكَرِ وَالْبَغْيِ ۚيَعِظُكُمْ لَعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ Hakika Allaah Anaamrishia uadilifu na ihsaan na kuwapa (mahitajio na msaada) jamaa wa karibu; na Anakataza machafu na munkari na ukandamizaji. Anakuwaidhini huenda mkapata kukumb...

Viungo vya Mwili vitashuhudia Matendo ya Mwanaadamu Siku ya Qiyaamah

Anasema Allaah  سبحانه وتعالى   ((الْيَوْمَ نَخْتِمُ عَلَى أَفْوَاهِهِمْ وَتُكَلِّمُنَا أَيْدِيهِمْ وَتَشْهَدُ أَرْجُلُهُمْ بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ)) ((Leo Tunaviziba vinywa vyao, na iseme Nasi mikono  yao , na itoe ushahidi miguu  yao kwa waliyokuwa wakiyachuma))  [Yaasiyn :65 ] Siku ya Qiyaamah viungo vya miili vitakuwa ni vyenye kushuhudia matendo ya binaadamu aliyoyatenda hapa duniani: Mfano mikono itasema: "nimeiba".  Miguu itasema, "nimekwenda sehemu ya ma'asi". Macho yatasema, "nimetazama machafu".  Masikio yatasema, "nimesikiliza nyimbo, au umbea" na kadhalika. Na hivi ndivyo itakavyokuwa hali ya makafiri, wanafiki na wenye kumuasi Mola siku ya kufufuliwa,  watakapokanusha madhambi waliyoyatenda duniani na kuapa kwamba hawakuyafanya, Allaah  سبحانه وتعالى  Atawafunga midomo  yao na kuviamrisha viungo vizungumze:   عن أنس بن مالك قال: كنا عند النبي صلى ال...